ELIMU YA MSINGI YA LISHE

UTANGULIZI

Mwili wa binadamu unahitaji lishe bora ili uweze kuwa na afya njema

LISHE NI NINI?

Lishe ni mchakato unaohusisha hatua mbalimbali za jinsi mwili unavyotumia chakula kilicholiwa ili kuupatia afya bora. Hatua hizi ni tangu chakula kinapoandaliwa, kinapoliwa jinsi mwili unavyokisaga na kukiyeyusha na hatimaye kufyonza virutubishi na kutumika mwilini.

CHAKULA NI NINI?

Chakula ni kitu chochote kinacholiwa na kuupatia mwili virutubishi mbalimbali kwa ajili ya afya bora. Chakula huupatia mwili nguvu na kuulinda dhidi ya maradhi mbalimbali. Mfano wa chakula ni Viazi, Wali, Ugali, nyama, Samaki, mchicha …

KAZI ZA CHAKULA MWILINI?

Mwili wa binadamu unahitaji nishati lishe(Nguvu) na virutubishi mbalimbali ili uweze kufanya kazi kwa ufanisi. Chakula tunachokula kinapaswa kutupatia Nishati lishe na Virutubishi  ambavyo hufyonzwa na kupelekwa sehemu mbalimbali za mwili kulingana na mahitaji ya mwili.

KAZI MUHIMU ZA CHAKULA MWILINI

  1. Kutengeneza seli za mwili na kukarabati seli zilizochakaa au kuharibika
  2. Kusaidia katika ukuaji wa mwili na ustawisho wa akili
  3. Kuupa mwili nguvu, joto na uwezo wa kufanya kazi
  4. Kuupa mwili kinga dhidi ya maradhi mbalimbali
  5. Kutengeneza vichocheo na vimeng’enyo mwilini
  6. Kusaidia katika utengenezaji wa maziwa ya mama

VIRUTUBISHI NI NINI?

Virutubishi ni viini vilivyoko kwenye chakula ambavyo vinauwezesha mwili kufanya kazi zake kwa ufanisi. Kila chakula kina uwezo wa kuupatia mwili baadhi ya virutubishi na huwezi pata virutubishi vyote ambavyo mwili unahitaji katika chakula kimoja isipokuwa maziwa ya mama kwa muda wa miezi sita ya mwanzo huweza kumpatia mtoto virutubishi vyote anavyohitaji.

Vyakula vyote vinaweza kuwa na kirutubishi zaidi ya kimoja ila kikatofautina na chakula kingine kwa kiasi na ubora, Mfano maziwa ya soya yanaweza kuwa protini zaidi kuliko nyama. Hivyo ni muhimu kula vyakula vya aina mbalimbali ili kuuwezesha mwili kupata virutubishi mchanganyiko vinavyohitajika.

MAMBO YA KUZINGATIA UNAPOKULA CHAKULA ILI KUPATA VIRUTUBISHI

  1. Ratiba ya mlo inayoeleweka; usile chakula mapema sana wala kwa kuchelewa bali uwe na ratiba inayoeleweka ya kupata chakula, kwani tumbo hufuata ratiba ambayo huwekwa na kuzingatiwa mara zote. Pia epuka kula chakula muda mfupi kabla ya kulala angalau mlo wa jioni uliwe masaa 2 kabla ya mtu kulala.
  2. Kiasi; Chakula kiliwe kwa kiasi kinachotosha kuondoa njaa na sio kupitiliza.
  3. Kula matonge madogo madogo; weka kiasi kidogo cha chakula kinywani ambacho unaweza kukitafuna vyema. Hii itasaidia kutafuna vyema chakula na kukichanganya na kilainishi(mate) na hivyo kumeng’enywa vizuri hasa kwa vyakula vya wanga
  4. Tulia na kula polepole; Kama una haraka ya kula ni vyema usile hadi utakapo tulia. Usile chakula ukiwa na haraka, hasira, wasiwasi na uchovu kwani inaweza kusababisha mchanyato tumboni.
  5. Tafuna vyema chakula; hii itasaidia kupata nishati lishe zaidi kutoka katika chakula kidogo.
  6. Usile vyakula aina nyingi kwa mlo mmoja; zingatia makundi ya vyakula angalau aina moja kutoka kwa kila kundi (aina tatu hadi nne zinafaa kwa mlo mmoja)
  7. Kula chakula kilichopikwa kwa urahisi na sio kilichowekwa vitu vingi kwani kinaweza kuwa chanzo cha mchanyato wa tumbo
  8. Kula aina tofauti ya chakula kwa kila mlo kama umekula ugali mchana, jioni kula viazi au ndizi
  9. Kula chakula ambacho kinaweza kumeng’enywa kwa urahisi, epuka vyakula vya mafuta sana na vyenye viungo vingi.
  10. Usinywe maji wakati wa kula, bali kunywa maji kati ya mlo na mlo au nusu saa baada ya kupata chakula ili kuruhusu umeng’enywaji wa chakula kufanyika kwa ufasaha.
  11. Kula matunda katika mlo mmoja na mboga za majani katika mlo mwingine, kasoro matunda jamii ya limao na machungwa yaweza liwa katika kila mlo.
  12. Jambo la kuzingatia ni kwamba unaweza kupumzika kabla ya chakula na kutembea tembea baada ya kupata chakula na si tofauti ya hapo, kwani watu wengi hupendelea kulala baada ya kupata chakula hii sio sawa kiafya.

Ili kupata afya bora tunapaswa kula chakula kilichoandaliwa katika hali ya usafi, upishi unaozingatia kutopoteza virutubishi na ulaji unaozingatia kanuni bora za afya.

Ttutaendelea na somo letu kujua aina za virutubishi na kazi zake mwilini.

Usisite kutembelea hii website kwa masomo zaidi.

Leave a Comment

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

 - 
English
 - 
en
French
 - 
fr
German
 - 
de
Portuguese
 - 
pt
Russian
 - 
ru
Spanish
 - 
es
Swahili
 - 
sw
swSwahili